Pages

Wednesday, 28 December 2016

AFARIKI BAADA YA WANANCHI KUUA NYOKA WAKE.

Mkazi wa Mtaa wa Mateka, Manispaa ya Songea, Denis Komba (26) kufa baada ya nyoka wake aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa jaketi kuuawa na wananchi.
Komba alifariki dunia katika hospitali ya Rufaa Songea mkoa wa Ruvuma (Homso) ambako alilazwa baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na fimbo nyoka wake huyo.
Mashuhuda wanaeleza kuwa kabla ya wananchi kumuua nyoka huyo, Komba aliwasihi wasifanye hivyo kwa kuwa wakimuua na yeye angekufa, lakini ombi lake hilo halikusikilizwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, siku ya tukio Komba alikodi pikipiki ya Kassian Haule (24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi, yenye namba za usajili MC 724 AKB ili apelekwe nyumbani kwake mtaa wa Mateka.
Akisimulia tukio hilo, alisema alipofika katika eneo la Benki ya Posta ya zamani barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alihisi kuna kitu kinamtekenya na kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo alipogeuka nyuma na kumwona abiria wake amebeba nyoka mkubwa huku amesimamisha kichwa.
Haule alisema, baada ya kumuona nyoka huyo aliruka kutoka kwenye pikipiki na kuanguka pembeni mwa barabara na abiria wake alimwachia yule nyoka ambaye alikimbilia kwenye kalavati la maji.
Aliongeza kuwa ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na kundi la vijana waendesha pikipiki wenzake walifika eneo hilo la tukio kwa lengo la kumsaidia mwenzao juu ya maswahiba yaliyompata hadi kumfanya apige kelele.
Alisema kabla ya vijana hao hawajafanya jambo lolote, Komba aliwaomba vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo wasimpige nyoka wake kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha. Kutokana na maneno hayo, Haule alimtoa nyoka huyo ndani ya kalavati na kwa kushirikiana na vijana wenzake walianza kumpiga nyoka huyo hadi kufa.
Alisema wakati wanampiga nyoka huyo, Komba ambaye ndiye mmiliki wa nyoka huyo naye alianza kulegea kisha akaanguka chini huku akitokwa na mapovu mdomoni na puani.
Habari zinasema kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari na wauguzi wa hospitali za kuokoa maisha yake zilishindikana kwani Komba alifariki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote na umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa Songea.
Alisema nyoka aliyeuawa na wananchi amechukuliwa na idara ya maliasili na uchunguzi zaidi ya tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini cha tukio hilo la kuuawa kwa nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa. Kamanda Mwombeji alisema, kwa upande wa dereva wa pikipiki yeye anaendelea vizuri na anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.
Aidha Kamanda Mwombeji, ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja kumiliki nyara za serikali.
#Jamii forums.

Wednesday, 26 October 2016

Rais Magufuli Ateuliwa kuwania tuzo ya Forbes kwa watu maarufu barani Afrika


Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameingia katika listi ya watu ambao wametajwa kuwania tuzo ya Person Of The Year 2016 ambayo hutolewa na Jarida la Forbes Africa.

Rais Magufuli ameingia katika kinyang’anyio hicho, akiwania tuzo hiyo pamoja na Mwanzilishi wa Capitec Bank, Michiel le Roux, Thuli Madonsela, Ameenah Gurib na watu wa Rwanda.

Kama Rais Magufuli atafanikiwa kushinda tuzo hiyo, basi Tanzania itakuwa imepata tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo kwani mwaka jana 2015, mshindi wa tuzo hiyo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji.

Utaratibu wa jinsi ya kupiga kura kwa mwaka huu ni kutumia tovuti yahttp://poy2016.com/ ambapo baada ya kuingia hapo, unaweza kugusa jina la mtu ambaye unapendekeza ashinde tuzo na hapo kura itakuwa imehesabiwa.

SOMA HABARI KTK MAGAZETI YA LEO O'CTOBA 26; 2016





















Friday, 21 October 2016

Serikali Yakubali Kurejesha Posho ya Sh. 8500 kwa Siku kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Nchini.




Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetuliza hasira za wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kurejesha posho ya chakula na malazi ya Sh8,500 kwa kila mmoja na kwamba tofauti baina yao itakuwa viwango vya ada.

Ufafanuzi huu uliotolewa jana usiku na Waziri wa Elimu, Sayansi , Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumza katika mahojiano maalimu na kituo cha runinga cha Taifa -TBC utakuwa faraja kwa wanafunzi ambao chini ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) walipanga kushinikiza walipwe posho ya Sh8,500 kwa siku kama ilivyokuwa awali. 
Hatua ya wanafunzi kujenga umoja ili kushinikiza haki katika posho ilitokana na baadhi yao kuingiziwa kati ya Sh40,000 na 70,000 badala ya Sh 510,000, hali ambayo ilizua sintofahamu. 

Ndalichako alisema tofauti ya malipo itakuwa katika ada na siyo posho, “Vigezo vya mikopo vimebadilika, kila mwanafunzi atapata fedha tofauti lakini tumefanya marekebisho kwenye posho ya chakula ambayo kila mwanafunzi atalipwa Sh8,500 kama awali.” 

Kwa mujibu wa utaratibu wa Bodi hiyo, malipo hayo ya chakula na malazi hutolewa kila baada ya miezi miwili. 

Mapema jana, Daruso iliwataka wanafunzi wa chuo hicho kutotia saini fomu za fedha za mikopo yao mpaka itakapowapa ruhusa ya kufanya hivyo. 

Rais wa Daruso, Erasmi Leon alisema hayo jana wakati akizungumza na wanafunzi wenzake kuhusu kusudio la kwenda HESLB kwa ajili ya kutafuta haki yao ya msingi. 

“Ninachowasihi tuwe pamoja. Tuwe wamoja na twende pamoja. Tutakwenda wawakilishi kutafuta nafasi kwa amani waweze kusikia tuna hoja gani lakini tukinyimwa hii nafasi tutaenda kuitafuta tukiwa wengi,”alisema na kuongeza:

 “Tuwe watulivu kwa sasa tutakapowahitaji muda na wakati wowote kwa lolote tushirikiane ili twende pamoja tumalize pamoja tuhakikishe tunapata Sh8,500 kwa kila mwanafunzi kwa chakula na malazi,”alisema. 

Kuhusu suala hilo, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ulisema wajibu wake ni kupokea na kusambaza majina na taarifa kutoka Bodi kwa wanafunzi. 

Akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi waliofika ofisini kwake kujua hatima yao na waliopata mikopo kuchukua fomu za kutia saini, Ofisa Mikopo wa UDSM, Lugano Mwakyusa alisema wenye jukumu la kujua walio na sifa ya kupata mikopo ni Bodi ya Mikopo. 

“Tunaendelea kupokea majina kutoka bodi. Tayari hapa kuna majina 949 yameshatoka, wengine tuzidi kusubiri na wale mwaka wa pili na tatu ambao walikuwa na mitihani ya marudio taarifa zao zitapelekwa bodi,”Mwakyusa aliwaambia wanafunzi waliokuwa wamejaa ofisini kwake.

 Kulikuwa na hali ya sintofahamu chuoni hapo jana baada ya wanafunzi wengi wa mwaka wa kwanza kuonekana wakiwa wameshika bahasha za kaki zilizokuwa na fomu za usajili wanazotakiwa kujaza huku wakihangaika kutokana na kutojua kiasi cha mkopo. 

Juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, AbdulRazaq Badru alieleza kwamba ingawa wanafunzi 88,000 waliomba mikopo kutoka HESLB, uwezo wa bodi hiyo ni kutoa kwa wanafunzi 21,500 pekee sawa na asilimia 24 na waliokuwa wameshapatiwa walikuwa 11,000 sawa na asilimia 12. 

Takwimu hizi zinaonyesha zaidi ya robo tatu ya wanafunzi wanaohitaji mikopo watakosa kutokana na uwezo mdogo wa kifedha. #source:Mpekuzi.com

MAGAZETI YA LEO IJUMAA OCTOBA 21,2016