Wednesday, 19 July 2017
Thursday, 13 April 2017
KASSIM MAJALIWA:AJIRA ZITOLEWE KILA ROBO MWAKA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza mamlaka ya serikali za mitaa, wizara na taasisi zote zitoe taarifa za ajira zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kila robo mwaka.
Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatano, Aprili 12, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati akitoa maelezo ya kuhitimisha majadiliano ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe ambaye aliitaka Serikali itoe maagizo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri kutengeneza ajira angalau 20,000 kila mwaka katika miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri zao, na taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo iwe inatolewa kila mwaka kwenye Bunge la Bajeti.
“Napenda, kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015, Ibara ya 59 inazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa zote nchini kuzingatia viashiria vya ukuzaji ajira katika mipango ya maendeleo ya ngazi husika pamoja na kutoa taarifa za mwenendo wa ajira kila robo mwaka,” amesema.
Waziri Mkuu amesema maelekezo hayo, yanazingatiwa katika Mwongozo wa kuandaa Bajeti ya Serikali unaotolewa na HAZINA kila mwaka ambao unazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi zote zibainishe fursa za ajira zinazotarajiwa kupatikana kila mwaka kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Vilevile mwongozo huo unazitaka taasisi hizo kutoa taarifa za ajira zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi hiyo kila robo mwaka. Ninatoa agizo, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi zote ziendelee kuzingatia maelekezo haya,” amesema.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa viwanda, Waziri Mkuu amesema ndani ya mwaka mmoja, jumla ya viwanda 2,169 vimesajiliwa vikiwemo viwanda vya mbolea, saruji, chuma na vya usindikaji wa mazao.
“Serikali pia inaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuvutia uwekezaji nchini. Uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda nchini ni dhahiri na tayari tumeanza kuona matokeo. Kwa mfano, mkoa wa Pwani peke yake una viwanda vikubwa 83 na vingine vidogo vidogo zaidi ya 200. Huu ndio mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama alisema Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Fedha Vijijini (MIVARF) ilipanga kukarabati barabara zenye jumla ya kilomita 148.5, kujenga masoko manne na kukarabati kituo kimoja cha mafunzo ya utunzaji mazao baada ya kuvuna.
Akijibu hoja za utekelezaji wa programu hiyo kwa upande wa Pemba na Unguja, Waziri Mhagama alisema miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara ilianza Agosti na Novemba 2014 na kazi hiyo kwa Pemba ilikamilika Desemba 2015 wakati kwa upande wa Unguja ilikamilika Januari 2016.
“Kazi za ujenzi wa masoko ya Kinyasini na Mombasa (Unguja) pamoja na Konde na Tibirinzi (Pemba) zilianza Desemba 2016 na zinatarajiwa kukamilika Julai 2017. Wakandarasi wamehimizwa kuhakikisha wanakamilisha kazi hizo katika muda uliopangwa ili kuendana na ratiba iliyopangwa,” alisema.
Akijibu hoja kuhusu uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma, Waziri Mhagama alisema uamuzi wa kuhamia Dodoma na kuifanya Makao Makuu ya Serikali ilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alitaka kuona Dodoma ikistawi na Serikali kuweza kuhamia huko ili kutekeleza kwa vitendo dhana ya Mji Mkuu.
Alisema uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma siyo suala la kisiasa kama baadhi ya watu wanavyodai bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili kama yalivyoelekezwa kwenye Ibara ya 151 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 na kama ilivyotamkwa kwenye GN namba 273 ambayo ni tamko la Serikali na sheria halali.
Naye Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Anthony Mavunde alisema kila mwaka vijana kati ya 800,000 hadi milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira wakati soko la ajira ni dogo.
Hata hivyo, Naibu Waziri Mavunde alisema Serikali imeanza kubadilisha mtazamo wa vijana kuhusu ajira kwani wengi wao hudhani kwamba kuwa na ajira ni lazima mtu avae tai, awe na ofisi yenye meza na kiti kinachozunguka.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Wednesday, 28 December 2016
AFARIKI BAADA YA WANANCHI KUUA NYOKA WAKE.
Mkazi wa Mtaa wa Mateka, Manispaa ya Songea, Denis Komba (26) kufa baada ya nyoka wake aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa jaketi kuuawa na wananchi.
Komba alifariki dunia katika hospitali ya Rufaa Songea mkoa wa Ruvuma (Homso) ambako alilazwa baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na fimbo nyoka wake huyo.
Mashuhuda wanaeleza kuwa kabla ya wananchi kumuua nyoka huyo, Komba aliwasihi wasifanye hivyo kwa kuwa wakimuua na yeye angekufa, lakini ombi lake hilo halikusikilizwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, siku ya tukio Komba alikodi pikipiki ya Kassian Haule (24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi, yenye namba za usajili MC 724 AKB ili apelekwe nyumbani kwake mtaa wa Mateka.
Akisimulia tukio hilo, alisema alipofika katika eneo la Benki ya Posta ya zamani barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alihisi kuna kitu kinamtekenya na kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo alipogeuka nyuma na kumwona abiria wake amebeba nyoka mkubwa huku amesimamisha kichwa.
Haule alisema, baada ya kumuona nyoka huyo aliruka kutoka kwenye pikipiki na kuanguka pembeni mwa barabara na abiria wake alimwachia yule nyoka ambaye alikimbilia kwenye kalavati la maji.
Aliongeza kuwa ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na kundi la vijana waendesha pikipiki wenzake walifika eneo hilo la tukio kwa lengo la kumsaidia mwenzao juu ya maswahiba yaliyompata hadi kumfanya apige kelele.
Alisema kabla ya vijana hao hawajafanya jambo lolote, Komba aliwaomba vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo wasimpige nyoka wake kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha. Kutokana na maneno hayo, Haule alimtoa nyoka huyo ndani ya kalavati na kwa kushirikiana na vijana wenzake walianza kumpiga nyoka huyo hadi kufa.
Alisema wakati wanampiga nyoka huyo, Komba ambaye ndiye mmiliki wa nyoka huyo naye alianza kulegea kisha akaanguka chini huku akitokwa na mapovu mdomoni na puani.
Habari zinasema kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari na wauguzi wa hospitali za kuokoa maisha yake zilishindikana kwani Komba alifariki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote na umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa Songea.
Alisema nyoka aliyeuawa na wananchi amechukuliwa na idara ya maliasili na uchunguzi zaidi ya tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini cha tukio hilo la kuuawa kwa nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa. Kamanda Mwombeji alisema, kwa upande wa dereva wa pikipiki yeye anaendelea vizuri na anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.
Aidha Kamanda Mwombeji, ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja kumiliki nyara za serikali.
#Jamii forums.
Wednesday, 26 October 2016
Rais Magufuli Ateuliwa kuwania tuzo ya Forbes kwa watu maarufu barani Afrika
Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameingia katika listi ya watu ambao wametajwa kuwania tuzo ya Person Of The Year 2016 ambayo hutolewa na Jarida la Forbes Africa.
Rais Magufuli ameingia katika kinyang’anyio hicho, akiwania tuzo hiyo pamoja na Mwanzilishi wa Capitec Bank, Michiel le Roux, Thuli Madonsela, Ameenah Gurib na watu wa Rwanda.
Kama Rais Magufuli atafanikiwa kushinda tuzo hiyo, basi Tanzania itakuwa imepata tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo kwani mwaka jana 2015, mshindi wa tuzo hiyo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji.
Utaratibu wa jinsi ya kupiga kura kwa mwaka huu ni kutumia tovuti yahttp://poy2016.com/ ambapo baada ya kuingia hapo, unaweza kugusa jina la mtu ambaye unapendekeza ashinde tuzo na hapo kura itakuwa imehesabiwa.
Subscribe to:
Posts (Atom)












































