KATIKA
sayansi ya mafanikio kuna mambo mengi sana yanahusika kutufikisha pale
tunapopataka.
Pia kuna njia tofauti zinazopendekezwa na wataalamu wa masuala ya
saikolojia. Mfano mwanafilosofia wa Ugiriki, Aristotle anasema:
“Binadamu ni kiumbe wa malengo.”
Pia kuna watu wanaweza wakahoji kwa nini tuwe na malengo katika maisha
yetu ya kila siku.
Zifuatazo ni sababu chache tu za kwanini tuwe na
malengo.
Kwa sababu mafanikio ni malengo na vingine vinafuata kwa hiyo kama
unataka mafanikio ya kweli inabidi uwe na malengo, bila malengo unakuwa
ni sawa na kisiwa chenye utajiri mwingi, lakini bado hakijavumbuliwa. kwa hiyo jitahidi uwe na malengo ikiwa ndiyo njia ya kufanikiwa.
Malengo ni kama mafuta katika safari ya kufanikiwa, umuhimu wa malengo
unafananishwa na mafuta katika gari kwani bila mafuta haiwezi kwenda, ni
sawa na malengo katika kazi hata kama una bidii sana kufanya kazi bila
malengo itakuwa vigumu kupima utendaji wako mwenyewe wa kazi wa kila
siku.
Malengo yanakusaidia kufikiria kile unachotaka, na kuwa na uwezo wa
kufikiria kile unachokitaka inakusaidia kuwa na nguvu ya ziada kuelekea
kupata yale unayoyataka katika maisha, ili uweze kufanikiwa ni lazima
uwe na maono ya kule unakoelekea.
Malengo yanakupa uwajibikaji kwa sababu mtu unakuwa unajua nini
unachokitaka au umepanga kufanikiwa nini kwenye sehemu yako ya kazi.
Malengo pia yanakusaidia kutumia muda vizuri ambao ni kitu muhimu katika
maisha, ukishindwa kutunza muda huwezi kufanikiwa.
Lakini vitu vya msingi ni kujifunza kwa mbinu tofauti ili tuweze kufikia
malengo.
Kwa mfano mwandishi mmoja anaitwa Brian Tracy, anaelezea umuhimu wa
malengo katika kitabu chake kinachoitwa Goals.
Anasema malengo ndio kitu pekee kinachosababisha mafanikio na jinsi ya
kuwa na mtazamo wa mbele kuelekea kile unachokitaka.
Kuna sababu nyingi sana za kwanini watu hawaweki malengo katika maisha
licha ya kuwa njia majawapo ya kufikia mafanikio.
Zifuatazo ni baadhi ya sabababu za kwanini watu hawaweki malengo.
Kuogopa kukataliwa kama kitu unachopanga kufanya watu watakikataa, hivyo
utajikuta unakata tamaa na kuhisi kukataliwa kihisia.
Hiyo inasababisha kuogopa kuweka malengo, hasa pale unapohisi utashindwa
kuyafanikisha, kwa ushauri tu jiamini, jipange na usije ukamwambia mtu
yeyote malengo na anza kuyatekeleza acha waone matokeo ya kile
unachokifanya.
Hofu ya kushindwa
Kushindwa kitu chochote kunaumiza na kunakatisha tamaa na msongo wa
mawazo. Lakini inabidi ujifunze kukabiliana navyo kwa sababu unapoanza
kitu chochote kipya ujue kuna changamoto zake.
Hapa namaanisha kwamba usije ukadhani unavyoanzisha kitu kipya utakutana
na urahisi, hapana kushindwa ni sehemu ya kujifunza.
Kutojua jinsi ya kuweka malengo
Watu wengi hawajui jinsi ya kuweka malengo wanafananisha malengo na
matarajio. Kwa mfano kuwa na familia yenye furaha na pesa nyingi hivi
kila mtu anavyo, malengo ni yale yaliyoandikwa kiufasaha na yanaeleweka
pia yakiwa na muda.
Pia watu wengi hawajui umuhimu wa kuweka malengo katika maisha, pia
familia nyingi hazina utamaduni wa kuwa na malengo, sasa basi jiwekee
utaratibu wa kuwa na malengo.
Malengo hayana umuhimu
Kama unaishi na watu ambao hawana malengo au familia ambayo
hawazungumzii umuhimu wa malengo ni kweli utafika umri wa utu uzima bila
kujua umuhimu wa kuweka malengo.
Ukiwa hujaweka malengo yoyote katika maisha ni bure. Wengi tuna
matarajio mengi bila ya kuwa na malengo.
Mara nyingi watu ambao hawana malengo ni wale ambao hawana furaha katika
kazi na ndoa zao, hii ni kwa sababu siri ya kupata furaha ya kweli ni kuwa na
mipango inayokuletea mafanikio.
Kabla hutujaangalia ni kwa namna gani ambavyo mtu unaweza kuweka
malengo, lazima tuelewe malengo ni nini hasa na yana sifa zipi.
Malengo lazima yaandikwe vizuri tena katika lugha nyepesi, pale
unapoyaandika yanakuwa yanajiandika kwenye moyo wako na kusababisha
uyakumbuka kila siku.
Malengo yawe rahisi kueleweka. Ina maana kwamba malengo ili iwe rahisi
kufikiwa ni lazima yawe rahisi kuelezea na ili lengo liweze kufanikiwa
ni lazima liwe na wazo moja la msingi likiwa ndilo wazo kuu na la msingi
katika lengo lako.
Kwa mfano ukiandika unataka kufanikiwa, ukaishia hapo bila kueleza
kwenye nyanja ipi, lazima uandike iwe ya kifedha au vinginevyo.
Malengo lazima yawe yamejieleza vya kutosha, mfano unataka kuongeza
kipato kwa kiasi gani kama ni 350,000 kwa mwezi lazima uandike unataka
kuongeza kipato kwa kiasi gani katika lengo lako kuu, usipoweka kiasi
mwisho wa siku utashindwa kujipima kama kweli umefikia lengo au la.
Na kisha ainisha ni kwa kiasi gani, itakusaidia kuweka mikakati ya jinsi
ya kufikia pale unapopataka.
Baada ya kuangalia jinsi malengo yanaweza kuandikwa, tuangalie ni jinsi
gani tunaweza kuweka malengo.
Angalia au chunguza tatizo ambalo linakuzuia kushindwa kufika pale
unapopataka na unawajibika kwa kiasi gani katika kutatua hilo tatizo,
kikwazo au changamoto inayokukabili.
Ukishajua tatizo linalokufanya uwe hapo ulipo na sio pale unapopataka
itakusaidia kuwa na mikakati na malengo ya jinsi utavyotatua tatizo au
jinsi ya kukabili changamoto ambayo unayo katika kufikia lengo.
Jione wewe mwenyewe kama ndio rais au mmiliki wa maisha yako mwenyewe,
hakuna yeyote anayehusika na kubadilisha hali ambayo unayo katika maisha
yako.
Acha kulaumu mtu yeyote kwa makosa yaliyojitokeza au matatizo, cha
kufanya ni kuchukua jukumu la kutatua tatizo kuliko kulalamika.
Kulalamika hakutatui tatizo ila kunakupunguzia uwezo wa kufikiria na
kutatua matatizo.
Hivyo basi, chukua hatua matatizo yanapojitokeza ili kujijengea uwezo wa
kiutendaji na uwajibikaji.
Punguza sababu pale unapokosea, zaidi jikite katika kutatua tatizo,
utajijengea misingi imara ya kuwa na malengo katika kazi zako za kila
siku na utakuwa na mchango chanya katika eneo lako la kazi.
Ukiwa unatoa sababu sana huwezi kuwa mtendaji mzuri na pia utakosa
mipango kwa sababu kila kitu unajitetea baada ya kuvaa uwajibikaji wa
jinsi ya kutatua tatizo.
Jione wewe ndio chachu ya mabadiliko katika maisha yako mwenyewe, kwa
sababu uko hapo ulipo kwa sababu ya uamuzi uliofanya na mipango
uliyoifanikisha na pia upo hapo kwa uamuzi na mipango uliyoshindwa
kuifikia.
Hivyo, weka mipango ya jinsi unavyotaka kuwa na kufanikiwa katika nyanja
ipi.
Kwa kuanzia sasa chukua uamuzi wa kumsamehe mtu yeyote aliyekukosea,
msamehe na usijadili tena mambo yaliyopita na weka malengo ya nini
unataka kufikia katika maisha yako.
Kwa mfano, kama umepunguzwa kazi usimlaumu bosi wako, kama umeonewa
jipange upya na anza kutafuta njia nyingine ya kuishi au kupata kazi,
usipende kujadili watu wanaokufanyia fitina za kukurudisha nyuma, cha
msingi weka mikakati ya kufikia malengo.