Pages

Wednesday, 18 November 2015

Jinsi walivyonusurika kufa,chakula chao ilikuwa Mende

HII NI MIUJIZA YA MUNGU
Wachimbaji wa watano wa madini kati ya sita waliodhaniwa kuwa wamekufa baada ya kufukiwa na kifusi Oktoba 5 katika machimbo ya Nyangalata wilayani Kahama, Shinyanga wameokolewa juzi wakiwa hai baada ya kuishi chini ya ardhi kwa siku 41.
Waliookolewa ni Mhangwa Amos, Joseph Bulale, Chacha Wambura, Onyiwa Awindo na Msafiri Gerald na sasa wamelazwa kwenye hospitali ya halmashauri ya mji wa Kahama kwa vile hali zao ni mbaya. Kwa muda wote wa siku 41 wameishi kwa kula wadudu, mizizi, magome ya miti na kunywa maji.
Mji wa Kahama ulikumbwa na taharuki juzi baada ya kuwapo wa taarifa za "kufufuka" watu hao kutokana na kutoamini iwapo wanaweza kuwa hai chini ya ardhi kwa siku 41. Kwa wengi ulionekana kuwa muujiza wa Mwenyezi Mungu kwani hata viongozi wa Serikali walishakiri kwamba isingewezekana kuwaokoa wakiwa hai.
Waziri asalimu amri
Oktoba 12, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga alisema juhudi za kuwaokoa zimeshindikana baada ya wataalamu kutoka kampuni ya Acacia Bulyanhulu kuchunguza na kubaini kuwa wachimbaji hao wamefukiwa umbali wa mita 120 kutoka usawa wa ardhi.
Kitwanga alisema kuwatoa watu hao ni kazi ngumu inayohitaji mitambo mikubwa yenye uwezo wa kufukua eneo lote la mgodi ili kuwafikia na kwamba kutokana na changamoto iliyopo, kazi hiyo inahitaji muda mrefu na wataalamu zaidi.
Juzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa mgodi huo wa Shigomico, Hamza Tandiko alisema ufukuaji ulihitaji gharama kubwa ambazo zilizidi uwezo wao hali iliyosababisha kuanza mkakati mpya wa kuwafukua watu hao, ambao tayari familia zao zilishatangaza msiba.
"Baada ya siku nyingi kupita tulijua tayari wamekufa. Tulipeleka msiba kwenye familia zao ikiwamo kuwapa fedha za rambirambi. Sisi huku tulianza kushirikiana na Serikali kujua jinsi ya kuopoa miili kwani uwezekano wa kuwapata hai ulikuwa mdogo," alisema Tandiko.
Hata hivyo, hakuna mitambo iliyokuwa imepelekwa wala watalaamu wowote, badala yake wachimbaji hao walihangaika peke yao chini ya ardhi hadi kujiokoa kwa kupenya maeneo mengine yanayoingiliana.
Simulizi walivyookolewa
Akisimuliza tukio hilo akiwa hospitalini jana alikolazwa na wenzake, mmoja wa wachimbaji hao, Chacha Wambura alisema; "Baada ya kukatika kwa kifusi hicho kiliziba njia ya kutokea, hali iliyowalazimisha kwenda kujificha kwenye kona ya mashimo hayo."
"Kwa kawaida mashimo ya wachimbaji, chini huwa na uwazi na njia mbalimbali ambazo hutengenezwa mfano wa vyumba ambavyo hutumika kuhifadhia mawe na vifaa vingine vya uchimbaji, hasa kutokana na urefu wa mashimo hayo ambayo mengine hufikia zaidi ya mita 100.
Mimi na wenzangu tulikwenda katika moja ya vyumba hivyo ndani ya mashimo na kuanza kutafuta njia ya kutokea, tukitumia mwanga wa tochi na simu za mkononi kabla hazijaishiwa moto.
Baada ya siku saba matumaini yalianza kufifia kutokana na kuanza kudhoofika kwa sababu ya njaa hivyo tukawa tunategemea kudra za Mwenyezi Mungu. Baadaye tuliona mwanga lakini ukiwa umezibwa na jiwe kubwa hali ambayo ilizidi kukatisha tamaa ya kuokoka, ingawa uliwasaidia kuona eneo lenye chemichemi ya maji yakitiririka.
Wakati huo, mwenzetu mmoja alizidiwa na sisi hatukutaka kumwacha hata mmoja, ilitubidi kuweka kambi eneo hilo tena huku tukimtaka ajikaze tutoke eneo hilo. Tulimsaidia tukawa wote eneo moja. Tulikuwa na kofia nzito za helmeti ambazo tulizitumia kukinga maji ingawa hayakuwa na ubora lakini tulikunywa hivyo hivyo," alisimulia Wambura.
Chakula ni magome na mende
"Tulikuwa tukitumia maganda ya miti inayofungwa kama nguzo kwenye mashimo yakawa chakula, wakati mwingine tulikamata wadudu kama vile mende lakini mwenzetu Mussa Supana aligoma kula akafa.
"Kadri siku zilivyosogea, hali ilizidi kuwa mbaya kwa sababu betri tulizoingia nazo pea nane ziliishiwa moto pamoja na betri za simu hali iliyosababisha kazi ya kujiokoa kufanyika gizani.
Kuna siku tulisikia sauti za wachimbaji wengine wakiendelea na uchimbaji kwenye mashimo mengine, lakini tulipopiga kelele za kuomba msaada, watu hao waliondoka moja kwa moja bila kutoa msaada hali iliyotufanya tuendelee kuishi kwa kula magome na wadudu tuliojua hawana sumu.
Siku ya kuokolewa tulisikia tena mtu mwingine akichimba dhahabu jirani na tulipokuwa, tulipopiga kelele ya kuomba msaada alituhoji sisi ni nani, tulipojitambulisha akasema tusubiri atoke nje. Baada ya muda tulianza kusikia milio na sauti ya wachimbaji wakitoboa njia mpaka wakatufikia tulipokuwa, ingawa mwenzetu tayari alikuwa amekufa."
Walazwa hospitali
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji Kahama, Dk Joseph Ngowi alisema hali zao zinaendelea vizuri ingawa kwa sasa hawawezi kula chakula kutokana na utumbo wao kusinyaa.
"Kwa kawaida mtu akiishi bila kula chochote na akiwa na afya nzuri anaweza kufa ndani ya siku 14, lakini hawa wamedumu kwa 41 kutokana na kula hao mende na magome ya miti na maji, lishe mwilini ilikwisha na walikuwa wakiishi kwa lishe ya protini ya misuli," alisema Dk Ngowi.
Alisema hali yao inaweza ikarudi baada ya siku saba na anashirikisha wataalamu mbalimbali wakiwamo wa lishe na mazoezi ya viungo kwani kutokana na kukaa sehemu finyu pamoja kwa siku nyingi, misuli imeshikana na inahitaji kufanyiwa mazoezi ya viungo.
Kaimu Kamishna wa Madini Tanzania, Ally Samaje alisema tukio hilo limewakuta wakiwa safarini kwenye machimbo hayo kwa lengo la kutaka kulifukua eneo hilo, lakini kabla hawajafika walipata taarifa kwamba watu hao wamefukuliwa.

Chanzo: #Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment