KAMPUNI za Pan Africa Power Solution
Tanzania Limited (PAP) na Independent
Power Tanzania Ltd (IPTL) na Harbinder
Singh Sethi, wamefungua kesi ya kikatiba
kupinga utekelezaji wa maazimio ya Bunge
yaliyotolewa kuhusu sakata la Akaunti ya
Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), inayodaiwa kuchotwa zaidi ya Sh
bilioni 300.
Kesi hiyo ilifunguliwa jana katika Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya hati
ya dharura dhidi ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru), Spika wa Bunge na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ilifunguliwa kupitia mawakili watatu wa
kampuni hizo, ambao ni Joseph Makandege,
Melchsedeck Lutema na Gabriel Mnyele.
Mawakili hao wanadai kwamba uamuzi
uliotolewa na Bunge, uliegemea upande
mmoja kwa vile baadhi ya wahusika
walioshiriki, ikiwamo Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Kabwe Zitto na Mbunge wa
Kigoma Kusini, David Kafulila wana kesi
kuhusu sakata hilo.
Pia, walidai kilichofanyika ndani ya Bunge
kuhusu sakata hilo ni kinyume cha Katiba
kwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria
alitafsiri vibaya amri halali, iliyotolewa na
Mahakama ya kuzuia mjadala huo usijadiliwe
bungeni.
Mawakili hao walidai kwamba mahakama
ilikusudia Bunge liweze kuendelea na
shughuli zake za kawaida wakati shughuli
nyingine zinazohusu maombi hayo
zikitekelezwa.
Miongoni mwa maazimio yaliyowasilishwa
bungeni ni kwamba Sethi, James Rugemalira,
Waziri wa Nishati na Madini na Katibu Mkuu
wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
walihusika kufanya miamala haramu ya
fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kwenda
kwa makampuni ya PAP na VIP Engineering
& Marketing.
Bunge liliazimia kwamba Takukuru, Jeshi la
Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na
usalama, viwachukulie hatua stahiki za
kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi, watu
wote waliotajwa na Taarifa Maalum ya
Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai
kuhusu miamala ya Akaunti ya Escrow.
Pia, bunge lilisema kutokana na vitendo vya
kijinai wanavyohusishwa navyo viongozi wa
umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini,
vinakiuka maadili na kuwanyima viongozi na
maofisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia
nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma
wa kuwawajibisha kwa kuishauri.
Hivyo azimio la pili Bunge liliwataka viongozi
hao akiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, wawajibishwe, kwa
kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua
uteuzi wao.
Katika azimio la tatu, Bunge liliazimia
kwamba Kamati za Bunge zichukue hatua za
haraka, kwa vyovyote kabla ya Mkutano wa
Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa
zao Wenyeviti tajwa wa Kamati husika za
Kudumu za Bunge; Pia, azimio la nne, Bunge
lilimtaka Rais Jakaya Kikwete aunde Tume
ya Kijaji ya Uchunguzi, kuchunguza tuhuma
za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius
Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, ambao
wanahusishwa katika kashfa hiyo.
Maazimio mengine yaliyotolewa na Bunge
kuhusu sakata hilo ni mamlaka husika za
kifedha na za kiuchunguzi, ziitaje Stanbic
Bank Ltd na benki nyingine
zitakazogundulika, kufuatia uchunguzi
uliofanywa na mamlaka za kiuchunguzi,
kujihusisha na utakatishaji wa fedha
zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa
ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa
fedha haramu.
Hata hivyo, Bunge liliitaka Serikali iandae na
kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya
Sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la
kuanzisha taasisi mahsusi
itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti
vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na
hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa
kiuchumi, kijamii na kisiasa; Vile vile, Bunge
liliaazimia kwamba Serikali iangalie
uwezekano wa kununua mitambo ya kufua
umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco
kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.
chanzo cha habari hii gazeti#habari leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment