Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akisaini kitabu cha wageni nchini Zambia mala baada ya kuwasili katika Ikulu ya Zambia kwa mazungumzo na mwenyeji wake Rais Edger Lungu (mwenye suti ya kijivu mbele ya Rais Kikwete)
Nchi ya Tanzania na Zambia zimekubaliana
kushirikiana kuimarisha sekta ya miundo mbinu hususani ya kufufua Reli
inayounganisha nchi hizi mbili (TAZARA) ili kukuza biashara na uwekezaji.
Makubaliano
hayo yamefikiwa jana wakati wa ziara ya siku mbili ya Rais wa Tanzania, Mhe.
Jakaya Kikwete nchini Zambia.
Akizungumza
wakati wa mkutano rasmi kati yake na mwenyeji wake, Mhe. Edgar Lungu, Rais wa
Zambia, Rais Kikwete alisema kuwa umefika wakati sasa wa kuifufua Reli
ya TAZARA ambayo ni kiungo muhimu na alama kubwa ya ushirikiano kati ya
Tanzania na Zambia.
Mhe.
Rais Kikwete alifafanua kuwa umuhimu wa reli hiyo ni wa kihistoria ambao
unahusisha nchi tatu za Tanzania, Zambia na Jamhuri ya Watu wa China ambao
kwa kiasi kikubwa walichangia ujenzi wa reli hiyo.
“Upo umuhimu mkubwa wa kuifufua Reli
ya TAZARA ili ifanye kazi kama awali kwani ni alama na kiungo muhimu cha
ushirikiano wetu sisi Tanzania na Zambia”, alisema Rais Kikwete.
Aidha,
aliongeza kuwa Tanzania na Zambia zimekubaliana kuwekeza zaidi katika reli
hiyo ikiwemo kuboresha uendeshaji na ukarabati ili kuirejesha katika hali
yake ya awali na hatimaye kukuza biashara na uwekezaji.
Alifafanua
kwamba hapo awali reli hiyo iliweza kusafirisha tani zaidi ya milioni 2 za
bidhaa kwa mwaka, wakati sasa reli hiyo inasafirisha tani laki 2 kwa
safari inayotumia hadi siku 12 kutoka Dar es Salaam hadi New Kapiri Mposhi
wakati malori yanatumia siku tano pekee.
“TAZARA inapita katika kipindi kigumu
sasa, hivyo tumezungumza namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili
ikiwemo uendeshaji na ukarabati ili irejee katika hali yake ya awali”,
alisisitiza Rais Kikwete.
Katika hatua nyingine Mhe.
Rais Kikwete alimpongeza Rais Lungu kwa kuchaguliwa hivi karibuni kuwa Rais
wa Zambia na pia alitoa salamu za pole kwa Rais huyo na Wazambia wote
kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Hayati Michael Satta.
Kwa upande wake, Rais Lungu alisema
kuwa Tanzania na Zambia zinajivunia mafanikio ya ushirikiano yaliyopo baina
ya nchi hizi mbili ambayo yamejikita katika sekta za Kilimo, Usafirishaji,
Nishati na Mawasiliano.
Pia, alisema kwamba nchi yake ipo
tayari kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo ambao unaanzia ngazi ya
serikali, kanda, Bara na Kimataifa na kusisitiza umuhimu wa kuitumia
Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 1992
kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa na
nchi hizi mbili. Aidha, alikubaliana na hoja ya kuifufua reli ya TAZARA kwa
manufaa ya nchi hizi mbili.
Rais Kikwete ambaye alikuwa nchini
humo kwa mwaliko wa Rais Lungu alifuatana na Mama Salma Kikwete, Mhe. Bernard
Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Saada Mkuya
Salum, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Charles Tizeba, Naibu Waziri wa Uchukuzi,
Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Grace Mujuma, Balozi wa
Tanzania nchini Zambia na Viongozi Waandamizi kutoka Serikalini na Mamlaka
mbalimbali.
|
Thursday 26 February 2015
Tanzania na Zambia kufufua Reli ya TAZARA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment