Pages

Thursday 17 September 2015

Umeme wa uhakika wiki hii-Tanesco

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema umeme wa uhakika utaanza kupatikana mwishoni mwa wiki baada mitambo ya kufua umeme ya Ubungo kuwashwa kwa ajili ya majaribio.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, jana, Msemaji wa Tanesco, Adrian Severin alisema kazi ya kuunga bomba la gesi kwenye mitambo ya kufua umeme ya Ubungo iliyoanza Julai 7, mwaka huu, ilikamilika juzi kama ilivyopangwa.

Alisema kazi hiyo ilianza baada ya gesi kutoka Mtwara kufika kwenye mtambo wa Kinyerezi.

Alisema baada ya gesi kufika kwenye mitambo ya Ubungo kinachofuata ni kuwashwa kwa ajili ya majaribio.

Alisema mtambo wa Ubungo I uliwashwa jana na leo utawashwa wa Ubungo II.

Mitambo hiyo ilizimwa wiki iliyopita ili kuunganisha bomba la gesi na kusababisha giza katika mikoa mbalimbali nchini inayopata umeme kutoka katika gridi ya taifa.

Aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi cha majaribio, akisema watarajie umeme wa uhakika.

Wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Felchesmi Mramba alikaririwa akisema wananchi watakuwa gizani kwa wiki moja ili kumaliza kazi hiyo.

Alisema gesi ya Mtwara inategemewa kuendesha mtambo wa Ubungo II wenye uwezo wa kuzalisha megawati 105, Symbion 112 na Kinyerezi I megawati 150.

Baadhi ya mikoa ambayo iko gizani kutokana na uunganishaji wa bomba la gesi ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Morogoro, Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Tabora, Shinyanga, Manyara na Zanzibar.

Waziri wa Nishati na madini, George Simbachawene aliwahi kukaririwa akisema, kukamilika kwa mradi wa umeme wa gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam utapunguza gharama ya nishati hiyo kwa wananchi.
#Chanzo-Mwananchi

No comments:

Post a Comment