Pages

Wednesday 2 September 2015

Mashehe waliotekwa DRC waachiwa

SERIKALI ya Tanzania kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimefanikisha jitihada za kuachiwa huru mashehe wa Tanzania waliokuwa wanashikiliwa mateka na moja ya vikundi vya uasi huko Kivu Kaskazini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula alisema kuwa taarifa za awali zinaeleza kwamba mashehe hao ambao walikwenda nchini DRC kwa ajili ya kuhubiri dini wameachiliwa huru na watekaji tarehe 01 Septemba, 2015.

Mulamula alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Congo, Mhe. Anthony Cheche, Inasema Mashehe hao kwa sasa wamepelekwa Mjini Goma ambako taratibu za kukutana nao na kupata undani wao zitafanyika kabla ya taratibu za kuwarejesha nchini kufanyika.


"Tumepokea taarifa hizo njema za kuachiliwa huru kwa mashehe hao jana kutoka kwa Balozi wetu nchini Congo na leo Balozi Cheche anatokea Kinshasa kwenda Goma waliko Mashehe hao ambapo tutajua idadi yao kamili na masuala mengine ya muhimu kutoka kwao yatajulikana kabla ya kuanza taratibu za kuwarejesha nchini" alisema Balozi Mulamula.

Aidha, Balozi Mulamula alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza Serikali ya Congo kwa ushirikiano wa hali ya juu waliouonesha hadi kufanisha Mashehe hao kuachiliwa huru wakiwa salama.

"Napenda kutoa rai kwa Watanzania wote wanaokwenda nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali kuwasiliana na Balozi zetu kwa kutoa taarifa zao ili wasaidiwe pale wanapopatwa na matatizo kwani ni jukumu la Balozi kulinda maslahi ya Tanzania na raia wake katika nchi wanayoiwakilisha, tumieni Wizara na Balozi zetu kwani ni jukumu letu", alisisitiza Balozi Mulamula.

Kwenye mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Haji Kombo alisema kuwa Serikali ya Zanzibar imefurahishwa na taarifa za kuachiliwa huru kwa mashehe hao ambao wanatokea Taasisi ya dini ya Tablighi ya Zanzibar.

"Tukio la kutekwa kwa mashehe hao lilikuwa la kushtusha na kufadhaisha, hata hivyo Serikali ya Jamhuri na ile ya Zanzibar zililichukua kwa uzito mkubwa kwa kuwa hawa ni Watanzania wenzetu na tunashukuru jitihada hizo zimezaa matunda kwa wenzetu hao kuachiliwa huru" alisema Balozi Silima.

No comments:

Post a Comment