Pages

Tuesday 15 September 2015

Rais ateua tena Wakuu wa Mikoa Wapya Wawili.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewateua wakuu wawili wapya wa mikoa kujaza nafasi zilizoachwa wazi na wakuu wa Mikoa ambao wanawania ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Septemba 14, 2015 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa katika uteuzi wake, Rais Kikwete amemteua Ndugu Amos Makalla kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Ndugu Jordan Rugimbana kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Aidha, Rais Kikwete amewahamisha wakuu wawili wa mikoa – Ndugu Mwantumu Bakari Mahiza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Ndugu Saidi Magalula ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akitokea Mkoa wa Tanga.
Ndugu Magalula anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Stella Manyanya anayewania ubunge mkoani Ruvuma pia.
Ndugu Makalla ambaye alipata kuwa Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Morogoro na Naibu Waziri wa Maji anachuku anafasi iliyoachwa wazi na ndugu Leonidas Gama ambaye anawania ubunge mkoani Ruvuma.
Ndugu Rugimbana ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Mahiza.
 Uteuzi na uhamisho huo ulianza Jumamosi, Septemba 12, mwaka huu, 2015 na wakuu wapya wa mikoa wataapishwa kesho kutwa Jumatano, Septemba 16, 2015, Ikulu, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Profesa Muhammed Bakari Kambi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Septemba 14, 2015 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa uteuzi huo ulianza tokea Jumatano, Septemba 9, 2015.
Kabla ya uteuzi wake, Profesa Muhammed Bakari Kambi alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Shirikishi cha Muhimbili, Dar es Salaam.
Vile vile, Rais Kikwete amemteua Ndugu Mlingi Elisha Mkucha kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC). Uteuzi huo ulianza Jumatano, Septemba 9, mwaka huu, 2015.
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Septemba 12, 2015 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Ikulu, Dar es Salaam imesema kuwa Ndugu Mlingi Elisha Mkucha ni mwanasheria kwa taaluma na mwajiriwa wa NDC kwa miaka 14 iliyopita ambako ametumikia katika nafasi mbali mbali mpaka akawa Kaimu Mtendaji Mkuu.
Ndugu Mkucha anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Gideon Nassari aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Dkt. Tulia Ackson kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia Jumatano, Septemba 9, mwaka huu, 2015.
Kabla ya uteuzi wake, Dkt. Tulia Ackson ni Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
 14 Septemba, 2015

















No comments:

Post a Comment