Pages

Sunday 6 September 2015

Sifa za kiongozi sahihi.

Habari za muda huu, bila shaka hujambo, leo nimeamua niilete hii mada kwenu ili kasumba iliyojengeka vichwani mwa watanzania iondoke na tuwe wapya, kasumba yenyewe ni hii ya kujua yupi kiongozi sahihi anayetufaa kwa manufaa yetu siyo kwa manufaa yake. 
Napenda nianike kwenu sifa za anayefaa kuwa kiongozi sahihi kwetu, sifa hizo za kiongozi sahihi ni zifuatazo:-
Awe ameelimika, 
hichi ndicho kigezo cha kwanza katika kumteua kiongozi anayetufaa katika jamii yetu. Mtu aliyeelimika hutufaa sana kuwa kiongozi siyo mtu aliye msomi, ndugu watanzania wenzangu tunapawa tujue tofauti kati ya msomi na aliyeelimika . Tunafaa kuongozwa na mtu aliyeelimika hata kama ameishia darasa la saba.
Kuongozwa na mtu msomi huku wengi wetu tukiona ni jambo bora haina manufaa kwetu, huyo msomi asiyeelimika alikuwa anasomea kujibu mtihani tu na si kusoma kwa ajili ya manufaa mengine. Tuepuke sana viongozi wa aina hii na tusijiaminishe kuwa msomi anafanya kitu sahihi pasipo kujua huyu mtu ameelimika, hili litatufanya tuwe na viongozi wenye kuongea maneno yasiyostahiki katika jengo letu tukufu.
Tunapaswa tumchague kiongozi mwenye hekima na busara katika maamuzi na kauli zake ndiyo anaweza kutufaa kwani ameelimika, mtu asiye na busara wala hekima hawezi kutufaa kutuongoza. Jengo lile tukufu lenye busati jekundu ndani yake halifai kuingiliwa na watu wasioelimika wenye kazi ya kuongea maneno yasiyostahiki kuongelewa na aliyeelimika, litakua kilabu cha pombe siyo jengo tukufu tena. Naomba tuliepuke hilo sana.

Aliye tayari kujitolea kwa wananchi wake, ndugu zangu pia tunatakiwa tuchague kiongozi aliyetayari kujitolea kwa wananchi wake na si kwa ajili ya maisha yawe mazuri. Kiongozi mwenye kujitolea hata kwa posho zake zikatwe ili kufidia jambo fulani dogo la kimaendeleo jimboni mwake ndiye anayehitajika na si kiongozi mwenye kukaa na kupiga kelele jimboni kwangu hakuna maji mara hakuna vifaa vya shule. Wakati yeye kiwanja chake anamilki kisima cha maji chenye kuweza kutatua tatizo la maji na ana uwezo kutengeneza kingine kama hicho bila kupiga hizo porojo akiwa ndani ya jengo tukufu. Huyo siyo kiongozi mwenye kujitoa wala msifurahie porojo zake huko ndani ya jengo, angalieni alijitolea kiasi gani akakwama ndiyo akapige kelele mule.

Awe na kihamasisho kitakachotuwezesha kumchagua. Ndugu watanzania wenzangu hapa namaanisha utendaji wake wa kazi hasa kwa mgombea urais, kihamasisho kinachohitajika yeye kuwa nacho ni utendaji wake wa kazi alivyokuwepo katika nyadhifa mbalimbali serikalini je unatufaa? Siyo kukaa na kuhadaiwa na kauli mbiu chache akiwa kwenye kampeni, kama alikuwa mbunge wa jimbo fulani tuangalie hilo jimbo lipo kwenye hatua gani tangu anakuwa mbunge hadi anafikia muda huo. Kama hakukuwa na mabadiliko yoyote huko jimboni kwake hadi muda huo tujiulizeni sehemu ndogo ya nchi imemshinda kimaendeleo je ndiyo nchi nzima ataiweza?
Kama alikuwa waziri wa wizara fulani tujiulizeni kafanya mangapi ya kutushawishi kwa kipindi chote hicho siyo tuje kuhadaiwa na vitu vya muda mfupi tutoe kura zetu halafu baadaye tuje kulia na kusaga meno. Kama aliwahi kuwa waziri mkuu tujiulize kwa muda huo wa miaka aliyowahi kukaa madarakani amefanya mangapi, alikuwa kiongozi mkuu wa shughuli za serikali utendaji wake unatushawishi vipi kumpa kura yetu. Alikuwa katibu mkuu wa baraza la mawaziri je utendaji wake ulikuwa vipi, siyo anatuahidi barabara nzuri wakati huo aliokuwa anaweza kumuhimiza waziri wa miundombinu akalitekeleza akiwa waziri mkuu. Tusiahidiwe, elimu bora, mikopo kwa wanafunzi, huduma bora za kijamii na mengineyo. Hayo yote aliweza kuyatekeleza akiwa waziri mkuu lakini hakuyatekeleza, je akiwa rais ambapo mshughulikiaji wake ni mtu mwingine atayaweza?
Hebu tuchekecheni bongo zetu kabla ya kutoa kura zetu, tusilete ushabiki wa kisoka kwenye maeneo haya.

Anayefanya mambo kwa matakwa ya wananchi wake na si kwa matakwa yake. Huyu ndiye kiongozi anayetufaa katika mfumo wetu uliopo nchini kwetu ingawa siyo mfumo wa ujamaa, tupo katika nchi yenye serikali ya wanachi na si serikali ya mtu mmoja hivyo maamuzi juu ya rasilimali za nchi au sekta ya uchumi ndani ya nchi yatokane na kauli za wananchi na si kauli ya kiongozi. Hivyo basi hata hawa wawakilishaji wa wananchi wa majimbo tuwape kura wenye kufuata matakwa yetu na siyo yao ili wakija kutoa kauli juu ya rasilimali zetu iwe ni kauli iliyotokana na sisi siyo iliyoyokana nao kwa manufaa yao.
Awe jasiri na mwenye kujiamini. Kiongozi pasipo kuwa jasiri na kujiamini ni sawa na bunduki isiyo na risasi, hawezi kuwaongoza wengine pasipo yeye kuwa jasiri na anayejiamini.
Muhimu: sifa tajwa hapo awali kabla ya hii ni lazima awe nazo.
#Toka:jamii forum"

No comments:

Post a Comment