Pages

Saturday 10 October 2015

MASHINE ZILIZOKAMATWA SIO ZA BVR WALA SIO ZA NEC

Ikiwa ni siku moja baada ya kunaswa mashine zilizosadikiwa kuwa ni za uandikishaji wapiga kura kwa njia ya kielektroniki (BVR), zilizokuwa zikiandikisha wafanyakazi wa Kiwanda cha MM Steel jijini Dar es Salaam, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeibuka na kueleza kuwa mashine hizo ni 'feki' na wala hazihusiani kwa namna yoyote na vifaa vyao.


Akitoa ufafanuzi huo Mkurugenzi wa NEC Ramadhani Kailima wakati akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na mashine hizo ambazo zilikamatwa juzi wakati zikiendelea kutumiwa kwa shughuli ya uandikishaji wa wafanyakazi wa kiwanda hicho kilichopo katika eneo la Mikocheni. 

 

Wakati Polisi wakizikamata jana kwa ushirikiano na maofisa kadhaa wa NEC, tayari mashine hizo zinavyofanana na BVR zilishaandikisha wafanyakazi zaidi ya 100 wa Kiwanda cha MM Steel.

 

Kailima alisema kuwa, mara baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa mashine hizo, walienda kuzikagua na kubaini kuwa hazina uhusiano na zile za Biometric Voter Registation (BVR), zilizotumiwa na wao (NEC) kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.

 

"Hakuna ukweli wowote kuwa zile ni mashine za BVR na tumebaini ni feki, tena ni sawa na zile zinazotumika kwenye ofisi mbalimbali kuandikisha wafanyakazi wake... hawa waliosema ni mashine za kuandikishia wapiga kura hawako sahihi... si kweli," alisema Kailima.

 

Alisema endapo watu wataendelea kuwa na shaka juu ya namna NEC inavyofanya kazi kwa sababu tu ya kuona mashine kama hizo, basi wanaweza pia kukamata mashine za ofisi nyingi zikiwamo za kwenye viwanja vya ndege, hospitali na hata manispaa kama ya Kinondoni ambayo hutumia mashine kama hizo kwa shughuli zake mbalimbali.

 

"Mashine tulizozikuta kwenye hiyo ofisi jana (juzi) ni computer mpakato (laptop) na mashine za kuchukua alama za vidole. Hata wale wafanyakazi tulipowahoji walibainisha kuwa wanazitumia kuorodhesha wafanyakazi wao kwa ajili ya usalama wa ofisi... na tena zipo ofisi nyingi zinatumia mashine hizo," alisema Kailima.

 

Kailima alitoa tahadhari kwa wataalamu wanaovishauri vyama vya siasa kuwa makini na kuacha kupotosha kwa kuwaleza mambo yasiyo na ukweli, hasa kuhusiana na NEC kwani wao wanafanya kazi zao kisayansi zaidi na hakuna fursa ya kuwapo kwa ubabaishaji wa aina yoyote.

 

Aliongeza kuwa hawafanyi kazi zao kwa misikumo ya kisiasa, bali huzingatia utaalamu na hivyo wanaotumiwa kwa ushauri na vyama waache kuwadanganya wanasiasa.

 

"Hawa wanasiasa wanadanganywa na watu wanaojiita wataalamu... mashine hizi (zilizokamatwa) hazihusiani na BVR," alisisitiza.

SOURCE:MICHUZIBLOG

No comments:

Post a Comment