Pages

Tuesday 13 October 2015

SABABU TATU ZILIZOSABABISHA WATU ZAIDI YA MILLION 1 KUKATWA DAFTARI LA WAPIGA KURA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza idadi mpya ya wapigakura ambayo ni milioni 22.75 baada ya uhakiki wa Daftari la Kudumu sambamba na kupungua kwa vituo kutoka 72,000 vilivyotangazwa awali mpaka 65, 105 baada ya kubainika kuwapo kwa zaidi ya majina milioni moja yaliyoandikwa kimakosa.

Mara baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, tume hiyo ilitangaza idadi ya walioandikishwa kuwa ni 23,782, 558.

Ikiwa imebaki wiki moja kabla ya daftari hilo kupelekwa vituoni kwa ajili ya uhakiki na utambuzi wa vituo vya kupigia kura kwa kila mwananchi, tume ikiwa kwenye mkutano na viongozi wa vyama vya siasa imetangaza marekebisho mapya yaliyopunguza idadi ya wapiga kura na vituo.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema kila chama kinapaswa kutoa elimu kwa wafuasi wake ili wakatambue vituo vyao vya kupigia kura siku nane kabla ya Uchaguzi Mkuu.

"Daftari la Kudumu la Wapigakura limekamilika. Baada ya uhakiki wa taarifa zote muhimu idadi kamili imepatikana. Watanzania 22, 751, 292 wa Bara watapiga kura mwaka huu kwenye vituo 63, 525 na 503,193 wa Visiwani watafanya hivyo kwenye vituo 1,580.

Tofauti inayojitokeza ni baada ya kufutwa kwa taarifa za wapigakura 1, 031, 769," alisema Jaji Lubuva.

Alibainisha sababu zilizochangia kufutwa kwa majina hayo baada ya uhakiki na uchakataji wa taarifa za wapigakura hao walioandikishwa wakati wa mchakato uliokamilika Oktoba mwaka huu.

Alizitaja sababu tatu na kutoa takwimu kwa kila moja. Watu 181, 452 walijiandikisha zaidi ya mara moja huku 3,870 waliandikishwa wakiwa si raia.

Wengine ni 845,944 waliojiandikisha wakati wa mafunzo kwa wataalamu, 74,502 walikuwa wanaandaliwa kuendesha mchakato huo kwa kila mkoa.

Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi (DIGP), Abdulrahman Kaniki aliwahakikishia viongozi hao kuwa jeshi lake limejipanga kukabiliana na uvunjifu wa amani.

Viongozi hao walilalamikia ukiukwaji wa sheria za uchaguzi ikiwamo ya wananchi kukaa umbali wa mita 200 kutoka kilipo kituo ili kusubiri matokeo.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema agizo hilo la NEC ni ukiukwaji wa sheria ya uchaguzi inayotoa ruhusa kwa wananchi kuwepo katika umbali huo wakisubiri matokeo.

Hata hivyo, Jaji Lubuva hakujibu hoja hiyo ya Mnyika bali alisisitiza kuwa wananchi watakapomaliza kupiga kura waende nyumbani.

Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama cha Umma (Chaumma) Taifa, Eugene Kabendera aliipongeza tume kwa maandalizi mazuri kuanzia uandikishaji mpaka utangazaji wa vituo lakini akatahadharisha kuhusu matokeo hasa ya urais.

Mwenyekiti wa chama cha APPT-Maendeleo, PeterMziray alisema ipo haja kwa wasimamizi wa uchaguzi kutendahaki wakati wakitekeleza majukumu yao.

#Mwananchi.

No comments:

Post a Comment