Pages

Friday 11 March 2016

Hatimae Rais atoa kibali Mawaziri wawili kusafari nje ya nchi

Rais Magufuli amewapa kibali mawaziri wawili kwenda Vietnam kujifunza mbinu za kuinua kilimo na kujenga viwanda ili kuwaondoa Watanzania kwenye lindi la umaskini.

Mawaziri wawili waliopata kibali hicho ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba.

Rais Magufuli alitoa uamuzi huo baada ya kufanya mazungumzo na Rais Truong Tang Sang wa Vietnam juzi na kukubaliana kuweka sawa mazingira ya biashara na uwekezaji baina ya nchi zao.

Akizungumza baada ya kumtembeza Rais huyo kwenye Eneo Maalumu la Uwekezaji la Benjamini Mkapa (EPZ) lililopo Ubungo jijini hapa, Waziri Mwijage alisema Dk Magufuli ametoa kibali hicho baada ya kuridhishwa na mabadiliko ya muda mfupi ya Vietnam.

"Kutokana na hatua waliyopiga, Rais ameniruhusu mimi na Waziri wa Kilimo, Mwigulu Nchemba kwenda nchini humo muda mfupi baada ya Rais Truong kuondoka.

"Nitakwenda kujifunza mbinu zao ili sekta ya viwanda iajiri zaidi ya asilimia 46 ya vijana wa Kitanzania," alisema Mwijage.
Baada ya kuondolewa vikwazo na Marekani, Vietnam ilichagua kuendeleza maeneo maalumu ya biashara na kufanikiwa kujijenga kiuchumi na kufikia uchumi wa kati katika kipindi cha miaka 23.

Aidha Rais Magufuli alizuia safari za nje siku chache baada ya kuapishwa akisema watumishi wa umma watakaokuwa wakitaka kwenda nje watalazimika kuomba kibali kutoka Ikulu, ikiwa ni mkakati wake wa kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali.

Tangu wakati huo, safari za nje kwa watumishi wa umma zimekuwa za nadra na mawaziri wamekuwa wakifanya ziara za kwenda mikoani kufuatilia utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment